SHIMA yapata Tuzo ya Mzalishaji Bora wa Maziwa Katika Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa 2025
Imewekwa: 02 Jun, 2025
SHIMA yapata Tuzo ya Mzalishaji Bora wa Maziwa Katika Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa 2025

Morogoro, Mei 31, 2025 – Shirika la Magereza (SHIMA) kupitia Kiwanda chake cha Kusindika Maziwa cha Kingolwira, kimetunukiwa tuzo ya Mzalishaji Bora wa Maziwa na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa yaliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, mkoani Morogoro.

Tuzo hiyo imetolewa kama kutambua mchango wa kiwanda hicho katika kuhakikisha uzalishaji bora na endelevu wa maziwa nchini. Mbali na kutunukiwa medali ya heshima, SHIMA pia imepokea keni nne (4) maalum za kuhifadhia maziwa kama sehemu ya zawadi ya tuzo hiyo.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, mwakilishi kutoka SHIMA alieleza kuwa heshima hiyo ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na Shirika hilo katika kuimarisha uzalishaji wa maziwa bora kupitia viwanda vyake, huku Kingolwira ikiwa miongoni mwa viwanda vinavyoongoza kwa ubora.

Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa inayolenga kuhamasisha uzalishaji, usindikaji na unywaji wa maziwa nchini, pamoja na kutambua mchango wa wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa maziwa.

TDB imesisitiza kuwa utoaji wa tuzo kama hizi unalenga kuongeza motisha kwa wazalishaji na kuchochea ushindani wa tija katika sekta ya maziwa.

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo