Dar es Salaam, 10 Disemba 2025 — Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Denis Lazaro Londo, leo amefanya ziara ya kikazi katika Kiwanda cha Magereza Ukonga, jijini Dar es Salaam, yenye lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za uzalishaji pamoja na kuangalia fursa za maboresho katika mifumo ya kiutendaji.
Katika ziara hiyo, Mhe. Londo alipokelewa na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es salaam SACP Mangala ambapo alipata maelezo ya kina kuhusu shughuli zinazofanyika kiwandani hapo, ikiwemo uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za magereza, mchango wake katika mapato ya Serikali, na hatua za kiusalama zinazotekelezwa.
Mhe. Londo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya kiwanda, kuongeza ubunifu na matumizi ya teknolojia ili kuongeza tija na ubora wa bidhaa zinazozalishwa. Pia alitoa wito wa kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Jeshi la Magereza na wadau wa maendeleo kwa ajili ya kupanua masoko ya bidhaa za viwanda vya magereza.
Aidha, Naibu Waziri alieleza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za Jeshi la Magereza katika kuhakikisha kwamba shughuli za uzalishaji zinakuwa endelevu na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika pato la taifa.
Ziara hiyo imehitimishwa kwa Mhe. Londo kutembelea baadhi ya maeneo ya kiwanda, kukagua mashine, vifaa vya uzalishaji pamoja na kukutana na watumishi waliopo katika maeneo mbalimbali ya kazi.

